Amorim ameinyoosha Man U na kuleta nidhamu - Luke Shaw
Eric Buyanza
August 1, 2025
Share :

Mlinzi wa Manchester United Luke Shaw amesema chumba cha kubadilishia nguo cha klabu hiyo kilikuwa “na sumu kali,” lakini kocha Ruben Amorim ameleta nidhamu mpya na mshikamano — hakuna tena nafasi kwa wachezaji wazembe.
Luke Shaw, amempongeza Amorim kwa kuchukua hatua kali kurekebisha hali ya hewa katika chumba cha kubadilishia nguo cha timu hiyo, akisema kuwa mazingira ya hapo awali yalikuwa "yamejaa sumu" na hayakuwa na afya kwa maendeleo ya wachezaji.
Amorim, ambaye aliteuliwa kuinoa United mwezi Novemba mwaka jana, amejipambanua kwa mtazamo usiokuwa wa kuyumbishwa: anataka nidhamu, kujituma, na wachezaji wanaoweka maslahi ya timu mbele.
Tayari amewatupilia mbali nyota kama Marcus Rashford na Alejandro Garnacho, miongoni mwa wachezaji watano waliotaka kuondoka klabuni katika kipindi cha uhamisho.
“Mara nyingi katika miaka ya hivi karibuni nikiwa hapa, hali imekuwa hasi kupita kiasi,” Shaw alisema. “Mazingira yanakuwa ya sumu kabisa, si yenye afya hata kidogo... tunahitaji mazingira yenye afya, chanya, yaliyojaa nguvu nzuri na furaha.”
Kwa mujibu wa Shaw, Amorim haangalii majina au hadhi ya mchezaji — anachotaka ni juhudi na ari ya kweli. “Ruben anaweka masharti makali. Mtazamo wa kisaikolojia ni jambo kubwa kwake... anataka asilimia 100 na hataki chochote pungufu. Mtu akifanya kazi kwa asilimia 85 au 90, hiyo haitoshi.” alisema.





