Kabila azungumza kwa mara ya kwanza tangu ahukumiwe kifo
Eric Buyanza
September 3, 2025
Share :

Rais wa zamani wa DRC, Joseph Kabila,amevunja ukimya kwa mara nyingine ikiwa ni majuma kadhaa kupita tangu ahukumiwe kunyongwa na mahakama mjini Kinshasa kwa madai ya kushirikiana na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda kuharibu usalama mashariki mwa nchi hiyo.
Kando na kuikosoa hukumu hiyo, Kabila amelaani hatua ya bunge la Senate kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa, suala analosema ni kinyume na katiba ya nchi.
Aidha Kabila amepinga tuhuma za ubakaji, mauaji, uhaini, uhalifu wa kivita, pamoja na kuwaunga mkono waasi wa AFC/M23, tuhuma anazosema hazina ushahidi wowote na zimechochewa kisiasa.
Katika taarifa yake rais Kabila amesema mashtaka yote yanayomkabili yanalenga kuunyamazisha upizani pamoja na kuwafungia wanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini Congo kushiriki siasa.
Mwezi uliopita bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani, majaji wa mahakama ya kijeshi walimhukumu rais Kabila kunyongwa kutokana na makosa ya uhaini.





