TRC yaanza kusafirisha makontena ya mizigo kwa SGR
Sisti Herman
February 20, 2026
Share :

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza usafirishaji wa makasha kwa kutumia reli ya Standard Gauge, hatua inayolenga kupanua wigo wa biashara, kupunguza msongamano wa mizigo bandarini na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda mikoa ya kati ya nchi.
Akizungumza wakati wa kuanza safari ya treni ya kwanza ya makasha kutoka Pugu kuelekea Ihumwa mkoani Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Usafirishaji wa TRC, Focus Makoye Sahani, amesema treni hiyo inasafiri umbali wa takribani kilometa 420 kutoka Dar es Salaam.
Amesema hatua hiyo ni mwanzo wa usafirishaji wa makasha baada ya TRC kuanza kusafirisha abiria pamoja na mizigo mbalimbali ikiwemo kichele kuanzia mwezi Julai, pamoja na saruji inayopakiwa Pugu.
“Leo tumeongeza wigo wa biashara kwa kupakia makasha. Kama mnavyoona, treni yetu ya kwanza ya makasha kwenda Ihumwa, Dodoma, leo imeanza safari zake na tuna ofa ya kutosha kutoka kwa mteja wetu wa kwanza,” amesema Sahani.
Ameeleza kuwa treni hiyo ina mabehewa 50 yanayobeba jumla ya makasha 100, huku mteja wa kwanza, GSM, akitoa ofa ya kuanzia kwa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa Sahani, TRC imeanza upakiaji wa makasha katika eneo la Pugu, huku ikifanya maboresho ya miundombinu ikiwemo Malindi Yard karibu na eneo la Gerezani ili kuimarisha shughuli za upakiaji wa makasha.





