Watoto 3 wa familia moja wafariki baada ya nyumba kuungua
Eric Buyanza
July 17, 2025
Share :
Watoto watatu wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wanaishi kuungua moto.
Watoto hao Membe Ndama (7), Mwaru Ndama (2)na Sayi Ndama (1)walikuwa wakiishi na wazazi wao katika Kijiji cha Nambilanje, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema kuwa tukio hilo limetokea jana Jumatano Julai 16, 2025 saa 11 jioni katika Kijiji cha Nambilanje.
Kamanda Imori amefafanua kuwa baba na mama wa watoto hao walitoka kwenda kuchota maji na kuchimba viazi hivyo waliwaacha watoto hao nyumbani, ambapo Sayi alikuwa amelala na wenzake walikuwa wakicheza nje ya nyumba hiyo.
"Hawa wazazi wa watoto waliofariki walikuwa wametoka na eneo walilokwenda lilikuwa siyo mbali na nyumbani. Baada ya muda kidogo waliona nyumba yao inaungua moto," amesema Kamanda Imori.
Amesema nyumba ilikuwa imeezekwa nyasi jambo lililosababisha kushika moto kwa haraka na kusababisha vifo vya watoto hao watatu.
Kamanda Imori amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni moto uliokuwa kwenye jiko la mawe kushika nyasi za ukuta wa ndani na kusababisha nyumba kuungua.
Miili ya marehemu hao imefanyiwa uchunguzi na Daktari Ezekia Ambekile wa Hosptali ya Wilaya ya Ruangwa na kubaini kuwa chanzo cha vifo ni kukosa hewa baada ya kuungua moto.
"Nimepokea miili ya marehemu muda wa jioni (jana) na kuifanyia uchunguzi kisha kugundua kuwa vifo vyao vilisababishwa na kukosa hewa," amesema Daktari Ambekile.
Baba wa marehemu hao, Ndama Mashauri (33) amesema kuwa wakati wanachota maji na mke wake Mindi Msasu (20) waliona moto unawaka nyumbani kwao na walipofika walikuta watoto wameshafariki.
"Nilitoka mimi na mke wangu kwenda kuchota maji na kuchimba viazi eneo kama la kilometa 2, tuliwaacha watoto nyumbani mmoja amelala na wawili walikuwa wanacheza, baadaye nikaona nyumba inaungua tulipofika karibu tuliwakuta watoto wetu wote watatu wamefariki dunia," amesema Mashauri.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuepuka tabia ya kuwaacha watoto peke yao bila uangalizi.
Mwananchi