10 watupwa jela kwa kuomba kurejeshwa kwa Utawala wa Kiraia
Eric Buyanza
June 25, 2024
Share :
Mali imewatupa jela wapinzani 10 wa serikali ya kijeshi, wakiwemo viongozi wa upinzani kwa kuomba nchi kurejeshwa chini ya utawala wa kiraia, mawakili wao waliliambia shirika la habari la AFP Jumatatu.
Mawakili wamesema watu hao 10, wakiwemo wakuu wa vyama vya siasa na makundi ambayo yalisaini tangazo la mwezi Machi wakiomba kurejea kwa demokrasia, wanashutumiwa kwa kufanya mikutano haramu na kupanga njama dhidi ya “mamlaka halali”.
Waliofungwa jela ni miongoni mwa watu 11 waliokamatwa na kuwekwa kizuizini wiki iliyopita wakati wakifanya mkutano wa faragha katika mji mkuu wa Bamako, baada ya kuomba kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Serikali ya kijeshi ilipiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa.
Upinzani umelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa “ukiukwaji mwingine wa haki msingi za uhuru,” unaofanywa na utawala wa kijeshi.
Viongozi wa kijeshi ambao walichukua madaraka mwaka 2020, waliahidi kuandaa uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa raia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, lakini baadaye waliahirisha uchaguzi huo kwa muda usiojulikana.