pmbet

Adaiwa kuua rafiki na kuchota milioni 61 kwenye akaunti yake

Eric Buyanza

July 12, 2024
Share :

Wakala wa Forodha, Mussa Bakari, maarufu Buda (30), anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salam kwa tuhuma za kuua rafiki yake Abdallah Selemani, kisha kuchota Sh. milioni 61 katika akaunti ya marehemu. 

Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa na kuhojiwa Juni 28 mwaka huu kuhusu tuhuma hizo.

"Tulimkamata na kumhoji kwa kina Mussa Bakari, Wakala wa Forodha, mkazi wa Temeke, mkoani Dar es Salaam, kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Selemani ambaye alikuwa rafiki yake.

"Baada ya kumuua, alifanikiwa kuiba fedha za marehemu Sh. milioni 61 kutoka katika akaunti ya huyo rafiki yake," alisema Kamanda Muliro.

Akisimulia zaidi kuhusu tukio hilo, kamanda huyo alisema kuwa Mei Mosi mwaka huu, saa 10:20 asubuhi, huko Mbutu Kichangani, Kigamboni, pembezoni mwa barabara itokayo Cheka kuelekea Beach ya Kichangani, uliokotwa mwili wa mwanamume akiwa ameshafariki dunia.

"Baadaye mwili huo ulitambuliwa kuwa ni wa Abdallah Selemani, mkazi wa Chanika, Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam," alisema.

Kamanda Muliro alisema kuwa Mei 4 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya kupotea kwa Abdallah zilizotolewa na mama yake, akieleza mtoto wake amepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Alisema uchunguzi wa Jeshi la Polisi baadaye uligundua kuwa Aprili 30 mwaka huu, mtuhumiwa Mussa alikuwa na marehemu wakitumia gari namba T 928 DFY, aina ya Suzuki Kei, wakitokea Magomeni kwenda Temeke Kijichi mpaka eneo ulipokutwa mwili huo.

"Uchunguzi wa vitu mbalimbali umebaini kuwa mtuhumiwa alimuua na baadaye kwenda kutupa mwili huo pembezoni mwa barabara ulikookotwa.

"Baada ya kumuua, mtuhumiwa alichukua kadi ya benki ya marehemu na kwa nyakati tofauti alitoa fedha Sh. milioni 61 kutoka katika akaunti ya marehemu," alidai Kamanda Muliro.

Alisema chanzo cha mauaji ni tamaa ya kutaka kuiba fedha kutoka kwa rafiki yake. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani muda wowote.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, ikithibitika Bakari alihusika na mauaji ya rafiki yake huyo kwa kukusudia, adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa. 

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet