Aenda jela miezi 3 kwa kuiba mahindi ya 'Buku Jelo'
Eric Buyanza
August 24, 2024
Share :
Jamaa mmoja huko nchini Kenya, aliyetambulika kwa jina la Meshack Opandiandiati, amehukumiwa na mahakama ya Kakamega ya nchini humo kwenda jela miezi mitatu kwa kosa la kuiba mahindi yenye thamani ya shilingi 70 za kenya (sawa na 1500 ya Tanzania).
Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Angeline Odawa ambapo alikiri mashtaka hayo.
Katika uamuzi wake, Bi Odawa alisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, akibainisha kuwa wizi, bila kujali kiwango kinachohusika, hauwezi kusamehewa.
“Wizi ni wizi, bila kujali umeibiwa kiasi gani. Sheria lazima iheshimiwe,” alieleza Hakimu.
Bwana Meshack alitozwa faini ya Sh10,000 (sawa na laki mbili za bongo) au kifungo cha miezi mitatu.
Katika kujitetea kwake mshtakiwa aliomba asamehewe kwasababu aliiba kutokana na njaa, hata hivyo, hakimu alisisitiza kwamba ingawa anaelewa changamoto za umaskini, lakini hazifai kuwa kisingizio cha uhalifu.
“Lazima tutafute njia bora za kukabiliana na matatizo yetu, lakini kuvunja sheria hakuwezi kuwa suluhu,” alisema.
TAIFALEO