Afisa UN auawa uvamizi Sudan, 52 wakiuwa, 64 wajeruhiwa
Sisti Herman
January 29, 2024
Share :
Wavamizi wenye silaha za moto wameshambulia vijiji siku ya jumamosi kwenye eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Abyei ambalo lina mzozo wa muda mrefu kati ya Sudan na Sudan Kusini, kila upande ukidai ni wao, huku uvamizi huo ukikadiria mauaji ya takriban watu 52, akiwemo mlinda amani wa Umoja wa Mataifa na majeruhi wanaokadiriwa kuwa 64.
“Madhumuni ya shambulizi hilo la Jumamosi usiku hayajabainishwa, lakini inashukiwa ni kutokana na mzozo wa ardhi,” Bulis Koch, ambaye ni waziri wa habari wa jimbo la Abiye, ameambia shirika la habari la AP kwa njia ya simu.
Ghasia zilizopelekea mauaji zimekuwa zikitokea mara kwa mara kwenye eneo hilo, ambako watu wa kabila la Twic Dinka kutoka jimbo jirani la Warrap wamekuwa kwenye mvutano wa ardhi na kabila la Ngok Dinka la Abyei, kutokana na eneo la Aneet karibu na mpaka.
Waliofanya mashambulizi ya Jumamosi walikuwa vijana kutoka kabila la Nuer ambao walihama kutoka jimbo la Warrap mwaka jana kufuatia mafuriko, ameongeza waziri Koch. Kupitia taarifa, kikosi cha muda cha UN, cha kulinda usalama katika eneo la Abiye, UNISFA, kimekemea shambulizi hilo ambalo limesababisha kifo cha mfanyakazi wake.