Afrika Kusini yafukuza wageni 2,745 ndani ya wiki moja
Eric Buyanza
June 15, 2026
Share :

Afrika Kusini imewarejesha nyumbani kwao wageni 2,745 ndani ya wiki moja kufuatia ahadi ya rais Cyril Ramaphosa ya kukabiliana na uhamiaji haramu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ametangaza siku ya Jumapili, Juni 14.
Rais Cyril Ramaphosa alikiri wasiwasi kuhusu uhamiaji haramu lakini alionya kwamba mamlaka haitamvumilia mtu yeyote kuchukua sheria mikononi mwake. Serikali ilibainisha kuwa wengi wa wale waliorejeshwa niwahamiaji wasio na vibali.
Nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na maandamano ya chuki dhidi ya wageni kwa miezi kadhaa.
Uporaji wa hivi karibuni wa biashara na mashambulizi yanayowalenga wageni umewafanya raia wa Nigeria, Malawi, Ghana, Zimbabwe, na Msumbiji kukubali programu za kuwarejesha nyumbani kwa hiari zilizoandaliwa na serikali zao.
Kamati ya wizara mbalimbali kuhusu uhamiaji imezungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili kutoa taarifa mpya kuhusu hatua zilizotekelezwa kupambana na uhamiaji haramu, kwani Waafrika Kusini wengi wamekuwa wakiandamana, wakati mwingine kwa vurugu, kwa miezi kadhaa, wakidai wahamiaji wasio na vibali waondoke nchini kabla ya Juni 30. Angalau raia wawili kutoka Msumbiji waliuawa; huko Durban, maelfu ya raia wa Malawi wamekusanyika katika kambi ya muda baada ya kutoroka vurugu, na nchi kadhaa, kama vile Ghana na Nigeria, zinaandaa kuwarejesha raia wao nyumbani.
RFI





