Afukuzwa kazi, kisa anatumia muda mwingi akiingia chooni
Eric Buyanza
December 29, 2025
Share :

Huko nchini China, mwanamume aliyefahamika kwa jina la Li, aliyekuwa akifanya kazi kama mhandisi kwenye kampuni moja Mkoani Jiangsu amemburuza bosi wake mahakamani kwa kumfukuza kazi kisa anatumia muda mrefu kila anapoingia chooni wakati wa masaa ya kazi.
Katika utetezi wake, kampuni hiyo ambayo haikutajwa jina iliwasilisha mahakamani picha za CCTV kama ushahidi zikimuonyesha Bwana Li kati ya Aprili na Mei 2024 akiingia chooni mara 14 ambapo moja ya safari hizo za chooni ilidumu kwa masaa 4.
Mhandisi huyo kwa upande wake, aliwasilisha mahakamani hapo dawa ya hemorrhoid ambayo mpenzi wake alimnunulia mtandaoni mwezi Mei na Juni mwaka jana, pamoja na rekodi za upasuaji kuanzia Januari 2025.
Yeye na mawakili wake walijaribu kuishawishi Mahakama kwamba mapumziko yake ya muda mrefu chooni yalikuwa halali kutokana na hali yake ya kiafya na kutaka Bwana Li alipwe Dollar elfu 45 (milioni 110 za kitanzania) kama fidia.
Kwa upande wa Mahakama ulidai kwamba ni kweli Bwana Li alikuwa akitumia muda mrefu chooni bila kutoa taarifa kwa muajiri wake kuwa ana tatizo la kiafya, jambo ambalo lingeweza kuishawishi kampuni hiyo impe likizo kwa ajili ya matibabu kama ilivyoelezwa kwenye mkataba wake wa ajira.
Jaji pia alibaini kuwa kampuni hiyo ilikishirikisha chama cha wafanyikazi kabla ya kumfukuza kazi Bwana Li.
Hata hivyo pande hizo mbili zilikubaliana kumaliza kesi hiyo huku kampuni hiyo ikikubali kumpa Bwana Li dola 4,200 (milioni 10) kama fidia kwa matatizo yake ya kifedha kutokana na kukosa ajira.





