Ahoua awaburuza wenzake kwa mabao Ligi Kuu
Eric Buyanza
June 4, 2025
Share :
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, anaongoza kwa kuhusika na mabao mengi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa.
Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa jana na Bodi ya Ligi, Ahoua, amehusika na mabao 23, akiwa ndiye kinara kwa kuhusika na idadi kubwa ya mabao kuliko mchezaji yeyote yule mpaka sasa.
Kiungo huyo aliyesajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Stella Club d'Adjame ya Ivory Coast, zamani ikiitwa Stella Abidjan, ndiye pia anayeongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu, akipachika 15 hadi sasa.
Kwa maana hiyo, Ahoua ametoa pasi za mwisho nane, ambazo zinamfanya kuhusika na idadi hiyo ya mabao.
Takwimu zinaonesha kuwa kwenye kikosi cha Simba, ndiye anaongoza pia kwa kuhusika na mabao mengi kuliko mchezaji mwingine yeyote, kwani mabao 63 ambayo timu hiyo imefunga, 23 amehusika nayo.
Pasi ya mwisho aliyoitoa, Jumatano iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Black Stars na kutumiwa vema na Steven Mukwala, akifunga bao pekee kwenye mchezo huo, ilimfanya kufikisha 'asisti' ya nane.
Kiungo huyo, anafuatiwa na straika wa Yanga, Prince Dube, aliyehusika na mabao 21, akifunga 13, kwenye nafasi ya pili ya ufungaji, akiwa na 'asisti' nane.
Pacome Zouzoua wa Yanga yeye anashika nafasi ya tatu, akihusika na mabao 18, akipachika nyavuni tisa na 'asisti' tisa pia, wakati Feisal Salum wa Yanga, akihusika na mabao 17.
Fei Toto ndiye kinara wa 'asisti' kwenye Ligi Kuu, akiwa nazo 13, huku akipachika mabao manne mpaka sasa.
Clement Mzize na Stephane Aziz Ki, wamehusika na mabao 16 kila mmoja, Mzize akiwa na mabao 13, asisti tatu, Aziz Ki, akifunga tisa, akiwa na asisti saba.
Wachezaji wa Simba, Stevan Mukwala na Leonel Ateba wamehusika na mabao 15 kila mmoja, Mukwala akiwa na mabao 12, asisti tatu sawa na Ateba ambaye ana idadi hiyo ya mabao.
NIPASHE