Ahukumiwa kifo kwa kuua watoto wa chekechea
Eric Buyanza
May 1, 2026
Share :

Mahakama nchini Uganda imemhukumu kifo Christopher Okello Onyum, mwenye uraia wa Uganda na Marekani kwa kuwaua watoto wanne katika shule ya chekechea mwezi huu kwa kuwachoma kisu, tukio lililozua hasira kwa umma na hofu kuhusu usalama wa wanafunzi nchini humo.
Tarehe 2 Aprili, Okello aliingia katika kituo cha kulelea watoto katika mtaa wa Ggaba akidai anataka kumsajili mwanawe. Hata hivyo, muda mfupi baadaye alifunga lango la kituo hicho na kuanza kuwashambulia watoto kwa kisu.
Tukio hilo lilizua mshtuko mkubwa ndani na nje ya Uganda. Kati ya watoto sita waliojeruhiwa, wanne walifariki papo hapo. Polisi walisema shambulizi hilo lilichukua muda mfupi, chini ya dakika saba, kabla ya kudhibitiwa.
Katika jitihada za kutuliza hasira za umma, rais Yoweri Museveni alielekeza kesi hiyo isikilizwe hadharani katika eneo la tukio. Kwa takribani wiki tatu, kesi hiyo imekuwa ikiendelea, huku mshtakiwa akikanusha mashtaka ya mauaji.
Mahakama ilieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa, ukiwemo wa wataalamu, ulithibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na akili timamu na alitekeleza tukio hilo kwa makusudi.
Uchunguzi wa simu na kompyuta yake pia ulibaini kuwa alitafuta mtandaoni maneno kama "shule zilizo karibu” na maudhui ya ukatili, hatua iliyotafsiriwa kuwa maandalizi ya awali.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutoa adhabu ya juu zaidi. Jaji Alice Komuhangi Kaukha alitoa hukumu ya kifo: "Ninahukumu kifo,” alisema jaji huyo, huku baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani wakishangilia uamuzi huo.
Hata hivyo, haijawa wazi mara moja kama adhabu hiyo itatekelezwa, kwani nchini Uganda utekelezaji wa hukumu ya kifo umesitishwa kwa muda mrefu, na waliohukumiwa mara nyingi hubadilishiwa kifungo cha maisha.
Mahakama ilieleza kuwa imezingatia uzito wa tukio hilo na athari zake kwa familia za wahanga, jamii ya eneo hilo pamoja na taifa kwa ujumla.
DW





