Aisha Masaka amwaga machozi kisa jeraha la goti kuzima ndoto zake.
Joyce Shedrack
July 1, 2025
Share :
Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania Twiga Stars anayekiwasha ligi kuu ya Uingereza katika klabu ya Wanawake ya Brighton Aisha Masaka ameweka wazi huzuni yake baada ya kushindwa kuliwakilisha Taifa katika michuano ya Afcon upande wa Wanawake kutokana na jeraha la goti alilolipata akiwa mazoezini.
Masaka ameandika ujumbe wa huzuni kupitia ukurasa wake wa Instagram huku akiweka wazi ukweli kuwa jeraha hilo la goti limezima ndoto aliyoitamani kwa muda mrefu.
“Ni vigumu kuelezea kwa maneno machungu ninayoyahisi sasa.Lakini itoshe kusema kwa ufupi michuano ya WAFCON ilikuwa ndoto niliyoitamani kwa muda mrefu – ndoto ya kuvaa jezi ya taifa langu na kupambana bega kwa bega na wenzangu kwa ajili ya bendera yetu”.
“Kwa bahati mbaya, majeraha ya goti niliyoyapata wakati wa maandalizi ya mwisho kuelekea fainali hizi, pamoja na mashindano ya CECAFA, yamezima ndoto hii. Ni maumivu makubwa sana kwangu – siyo tu kimwili, bali zaidi kiakili na kihisia – kwa sababu najua ni jambo nililoliombea na kulifanyia kazi kwa muda mrefu”
“Lakini naamini kila jambo hutokea kwa sababu, na mapenzi ya Mungu daima ni makubwa kuliko mipango yetu Binadamu. Nitaendelea kupigania kupona na kurejea uwanjani nikiwa na nguvu mpya, moyo mpya, na ari kubwa kuliko awali”
“Ninawashukuru kwa dhati mashabiki, familia, marafiki na wenzangu kwa sala, upendo na maneno yenu ya kunitia moyo. Sapoti yenu inanipa sababu ya kuendelea kusimama imara na kutokata tamaa”
“Naamini wachezaji wenzangu wataendelea kupambana kwa moyo wote na kulitumikia taifa letu kwa fahari kubwa, kama walivyofanya kwenye michuano ya CECAFA. Let’s go Twiga Stars! @twigastarz 💪🏾💪🏾💪🏾”.
"Watanzania wote tuko nyuma yenu, tunawatakia kila la heri na mafanikio kwenye michuano hii asanteni sana 🌻🩷🙏🏾".