Ajali ya basi yaua watu wanne Tabora
Sisti Herman
August 24, 2026
Share :

Watu wanne, wakiwemo Watoto wawili wamefariki dunia baada ya basi la Kampuni ya Miza Express lililokuwa likitoka Mpanda kuelekea Bariadi kupata ajali katika eneo la Kijiji cha Ngukumo, Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 9 usiku, baada ya basi hilo kuacha njia na kutumbukia bondeni, kilomita chache kabla ya kufika Makao Makuu ya Wilaya ya Nzega.
Baadhi ya Abiria walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya matibabu, huku wengine waliokuwa wamenasa ndani ya basi wakilazimika kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Twawa Juma Lulengelule amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema waliofariki ni Wanaume watatu na Mwanamke mmoja.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni Dereva kukosa umakini na kushindwa kulimudu basi, ambalo lilitoka nje ya barabara, kugonga vyuma vya kingo za barabara na kisha kupinduka na kutumbukia bondeni.





