Ajitolea kuwapelekea wanyama maji mbugani baada ya ukame
Eric Buyanza
April 22, 2026
Share :

Patrick Kilonzo Mwalua kutoka nchini Kenya alijitolea maisha yake kwa kuamua kusafirisha maelfu ya lita za maji kwa wanyamapori ambao walikuwa wako kwenye hatari ya kufa kwa kiu.
Kwa huruma yake alijegeuza kutoka mkulima wa mbaazi hadi kuwa mhifadhi na aliendelea kuifanya kazi hiyo hata alipokuwa kwenye kitanda cha hospitali siku chache kabla ya kufa akiwa na umri wa miaka 54.
Patrick alisukumwa kufanya kazi hiyo baada ya kumuona nyati akianguka kutokana na kiu.
JINSI ILIVYOANZA
Mwaka 2016 ukame mkali ulipoifanya Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo Magharibi ya Kenya kuwa bakuli la vumbi, Mwalua alianza kuendesha lori kwenye eneo korofi ili kupeleka lita 3,000 za maji kila siku kwa ajili ya tembo, pundamilia na swala waliokaukiwa.
Kazi yake hiyo ya kujitolea ambayo ilinaswa na camera za vyombo vingi vya habari duniani, iliwaonyesha wanyama wakilikimbilia lori la Patrick pale alipokuwa akiwasili mbugani.
Watu kutoka maeneo mbalimbali duniani walijitolea kumuunga mkono "Mtu wa Maji wa Tsavo," wakitoa michango ili kuokoa maisha ya wanyama.
Ahadi ya Mwalua kwa wanyamapori ilikuwa kamili, hata kama afya yake mwenyewe ilidhoofika.
Licha ya kupata tatizo la figo na kuhitaji kusafishwa damu mara kwa mara lakini alisimama imara akatoka kwenye kitanda cha hospitali ili kuratibu utoaji wa maji.
Ingawa baadae alifariki lakini mke wake Rachel na Shirika la Wanyamapori la Mwalua wanaendelea na kazi hiyo muhimu hadi leo.





