Akaa gerezani miaka 48 kwa kosa ambalo hakufanya!
Eric Buyanza
December 23, 2023
Share :
Mwanaume mmoja huko nchini Marekani ameachiliwa huru baada ya kukaa gerezani kwa miaka 48, baada ya kubainika kuwa hakuwa na hatia kutokana na mashtaka ya mauaji yaliyokuwa yakimkabili.
Glynn Simmons, 71, aliachiliwa baada ya viongozi wa mashtaka kukubali kwamba ushahidi uliotolewa dhidi yake haukuthibitisha kwamba alishiriki kwenye mauaji hayo.
“Baada ya uchunguzi wa kina, mahakama hii imebaini kwamba ushahidi uliowasilishwa dhidi ya mshtakiwa haukumhusisha kwa vyovyote vile na mauaji aliyokabiliwa nayo,” akasema Jaji Amy Palumbo.
Simmons amekaa gerezani kwa jumla ya miaka 48, mwezi mmoja na siku 18, hilo linamfanya kuwa mahabusu aliyezuiliwa kwa muda mrefu zaidi nchini Marekani.
Simmons alifungwa gerezani mwaka 1975, na alikuwa na umri wa miaka 22 wakati huo yeye na mshtakiwa mwenzake, Don Roberts, walipopatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.