Alala maskini na kuamka tajiri baada kupata almasi ya milioni 257
Eric Buyanza
July 25, 2024
Share :
Maisha Raju Gound yamebadilika ghafla baada ya kupata almasi kubwa katika mgodi wa Madhya Pradesh huko nchini India.
Almasi hiyo ya karati 19.22 inatarajiwa kuuzwa katika mnada wa serikali kwa Dola 95,570 (sawa na milioni 257 za kibongo).
Raju alisema amekuwa akikodisha migodi katika jiji la Panna kwa zaidi ya miaka 10 kwa matumaini ya kupata almasi bila mafanikio yoyote, na baba yake alikodisha mgodi huo miezi miwili iliyopita.
"Sisi ni maskini sana na hatuna chanzo kingine cha mapato. Kwa hiyo tunafanya hivi kwa matumaini ya kupata chochote," alisema.
Siku ya Jumatano asubuhi, alienda kwenye mgodi huo kufanya kazi yake ya kila siku ya kutafuta jiwe hilo la thamani.
"Ni kazi ya kuchosha. Tunachimba shimo, tunatoa udongo na vipande vya mawe, kuvichakata kwenye ungo na kisha kuchuja kwa uangalifu maelfu ya vipande vya mawe viliyoshikana kutafuta almasi," alisema.
Na siku hiyo, kazi hiyo ngumu ilizaa matunda yatakayobadilisha maisha yake .
“Nilikuwa nikipekua mawe nikaona kitu mithili ya kipande cha glasi, niliinua macho yangu na kuona mwanga, ndipo nilipojua nimepata almasi,” alisema.
Baada ya ugunduzi huo Bw Gound alipeleka bidhaa yake kwenye ya serikali ambapo ilitathminiwa na kupimwa.
Bw Singh, afisa katika ofisi ya almasi ya serikali anasema almasi hiyo itauzwa katika mnada ujao wa serikali na kwamba Bw Gound atapokea pesa yake baada ya mrahaba na ushuru wa serikali kukatwa.
Bw Gound anatumai kujengea familia yake nyumba nzuri na kulipia masomo ya watoto wake. Lakini kwanza, anataka kulipa deni lake la rupee 500,000.