Aliyemuua mumewe kwa kisu cha mgongoni apandishwa kizimbani
Eric Buyanza
June 11, 2024
Share :
Beatrice Elias (36), mkazi wa Katanini, Kata ya Karanga katika Manispaa ya Moshi, amepandishwa kizimbani akikabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya mume wake, Evagro Msele.
Msele (43) aliyekuwa mfanyabiashara maarufu katika mji wa Moshi, aliuawa Mei 25, mwaka huu kwa kuchomwa kisu mgongoni, akiwa nyumbani kwa mtu anayedaiwa kuwa mzazi mwenzie.
Mshtakiwa alifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Herieth Mhenga.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Hendry Daudi, alidai kuwa kesi hiyo namba 15731 ya mwaka 2024 inayomkabili Beatrice, upelelezi wake haujakamilika.
Msele, aliuawa Mei 25 mwaka huu, majira ya saa 3:50 usiku na mtu anayedaiwa kuwa mkewe wa ndoa, katika eneo la Pumuwani A, Kata ya Kirua Vunjo, Wilaya ya Moshi, baada ya kumkuta nyumbani kwa mwanamke mwingine.
Beatrice ameshtakiwa kwa kosa la mauaji, chini ya kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura 16 ya Sheria hiyo iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Baada ya kusomwa maelezo hayo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote, kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 25, mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.
NIPASHE