Aliyepandikizwa figo ya nguruwe atoka hospitali
Eric Buyanza
April 4, 2024
Share :
Mwanaume wa kwanza kupandikizwa figo ya nguruwe ameruhusiwa kutoka hospitali, ikiwa ni wiki mbili baada ya kufanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Massachusetts nchini Marekani.
Katika siku za nyuma upandikizaji wa viungo kutoka kwa nguruwe waliobadilishwa vinasaba ilikuwa ni jambo lisilowezekana kutokana na majaribio mengi kufeli, lakini mafanikio haya yamepongezwa na wanasayansi kote ulimwenguni.
Katika taarifa, hospitali hiyo ilisema mgonjwa, Richard "Rick" Slayman alikuwa akipambana na ugonjwa wa figo na alihitaji kupandikizwa kiungo hicho ili kuokoa maisha yake.
Madaktari walifanikiwa kupandikiza figo ya nguruwe iliyobadilishwa vinasaba katika mwili wake katika upasuaji uliofanyika kwa masaa manne tarehe 16 mwezi Machi.
Taarifa iliendelea kusema kuwa figo ya Bw Slayman sasa inafanya kazi vizuri na kwamba hahitaji tena kufanyiwa tiba ya dialysis (kusafishwa damu).