Aliyepoteza mikono yote 2 kwenye ajali, apandikizwa mipya
Eric Buyanza
March 8, 2024
Share :
Raj Kumar aliyepoteza mikono yote miwili amefanikiwa kupewa mikono mipya kupitia upasuaji uliofanikiwa sana katika hospitali ya Ganga Ram mjini Delhi nchini India.
Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 45 alikuwa mchoraji ambaye alipoteza mikono yake yote miwili katika ajali ya treni mwaka 2020.
Mikono hiyo ilitolewa na mwanamke aitwaye Meena Mehta, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Utawala wa Shule maarufu Kusini mwa Delhi na mwanamke huyo aliahidi kutoa baadhi ya viungo vyake kwa wenye uhitaji baada ya kifo chake.
Hapo awali, figo, ini, na sehemu za macho za Meena Mehta zilibadilisha maisha ya wagonjwa wengine watatu, na sasa mikono yake imetumika tena kuongeza matumaini kwa mchoraji huyo.
Taarifa zinasema upasuaji huo mgumu ulichukua zaidi ya masaa 12, na baada ya upasuaji huo kufanikiwa timu ya madaktari ilipiga picha ya pamoja na mgonjwa aliyeonekana akitoa ‘dole gumba’ akiwa na mikono yake mipya aliyopandikizwa.
Mgonjwa huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini jana Machi 7.