Aliyetumbuliwa kisa vipimo vya Corona, arejeshwa kazini
Eric Buyanza
April 12, 2024
Share :
Ikiwa ni miaka mitatu na miezi 11 tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL) Dk. Nyambura Moremi, kuondolewa katika nafasi hiyo ili kupisha uchunguzi baada ya kubainika kasoro za kiutendaji, amerejeshwa katika nafasi hiyo.
Mei 3, 2020 aliyekuwa Rais, Hayati Dk. John Magufuli, wakati akimwapisha Waziri wa Katiba na Sheria, alibainisha changamoto za utendaji wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alichukua hatua.
Siku hiyo hiyo, Waziri Ummy kupitia taarifa yake kwa vyombo vya Habari, alimwelekeza aliyekuwa Katibu Mkuu (Afya) kuwasimamisha kazi mara moja Dk. Moremi na Jacob Lusekelo, Meneja Udhibiti wa Ubora ili kupisha uchunguzi.
Kadhalika, aliunda kamati ya wataalam wabobezi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa NPHL ikiwamo mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za UVIKO-19.
Kamati ilipewa kazi hiyo na kutakiwa kuikamilisha Mei 13, 2020 ili kuwasilisha taarifa kwa waziri husika.
Magufuli alionyesha shaka kuhusu ufanisi wa maabara hiyo baada ya kupima sampuli za matunda na wanyama na baadhi kukutwa na maambukizi ya UVIKO-19.