Amadu Koita aenda jela miaka 182 kwa kutaka kupindua serikali
Eric Buyanza
July 23, 2024
Share :
Mahakama nchini Sierra Leone imewakuta na hatia watu 11 wanaotuhumiwa kwa uhaini na makosa mengine baada ya jaribio la mapinduzi mwezi Novemba mwaka jana.
Miongoni mwao ni Amadu Koita Makalo, mwanajeshi wa zamani, aliyekuwa mlinzi wa aliyekuwa Rais Ernest Bai Koroma, ambaye Mahakama imemhukumu miaka 182 jela.
Koita Makalo alikuwa na ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kuikosoa serikali ya Rais Julius Maada Bio, huku serikali ikimtuhumu kuwa miongoni mwa watu waliopanga jaribio hilo la mapinduzi.
RFI imeripoti kuwa mbali na Makalo, watu wengine 10 ambao wamepatikana na hatia hiyo, bado wanasubiri kufahamu kifungo kinachowakabili kwa mujibu wa msemaji wa Mahakama.
Tarehe 26 mwezi Novemba mwaka jana, watu wenye silaha walivamia kambi mbili za kijeshi, magereza mawili na vituo viwili vya polisi na kukabiliana na maafisa wa usalama, katika tukio ambalo serikali ilisema lilikuwa ni jaribio la mapinduzi.
Watu 21 waliuawa na mamia ya wafungwa walitoroka wakati wa tukio hilo.