Ambaka mtoto wake ili apate utajiri
Eric Buyanza
December 22, 2023
Share :
Jeshi la Polisi mkoani Geita limefanikisha kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha maisha mkazi wa Kijiji cha Shinyanga A wilayani Mbogwe, Mabula Maduhu (23) aliyetuhumiwa kumbaka mwanaye.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Safia Jongo amesema hayo Desemba 21, 2023 mbele ya waandishi wa habari na kueleza mtuhumiwa alikutwa na hatia na kuhukumiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbogwe.
Amesema kiini cha Maduhu kutenda ukatili huo ni imani za kishirikina ambapo aliamini kuwa akifanya kitendo hicho atapata utajiri ndipo jeshi la polisi lilimkamata, kufanya upelelezi na kisha kumfikisha mahakamani.
Kamanda ameeleza kesi hiyo ni miongoni mwa kesi 157 ambazo zimepata mafanikio mahakamani kati ya kesi jinai 423 zilizoripotiwa na kupelekwa mahakamani kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2023.