Ameshindwa kuibadili yanga, wameamua kumbadili yeye
Eric Buyanza
May 7, 2026
Share :

Imefika mwisho. Mtaani huwa tunasema hivyo. Ndoa ya Yanga SC na kocha Pedro imefikia mwisho jana jioni dakika chache lilipomalizika pambano lao na KMC pale KMC Stadium. Hakuna unachoweza kubadili.
Muda mrefu mahusiano ya Pedro na Yanga SC yalikuwa shakani.
Kilichokuwa kinafanyika ni Pedro kuwaibia muda wao Yanga SC, huku Yanga SC wakiamini Pedro angeirudisha timu yao katika makali yake. Yanga SC walishikwa hapa na Pedro.
Walimpa muda wakiamini timu yao itarudi kule kwa kina Gamondi, Ramovic na Professa Nabi.
Waliamini hilo litaenda kutokea. Haikuwa hivyo, maisha yakaendelea kubaki vile vile.
Timu ikaendelea kucheza inavyocheza. Yanga SC wakamuongeza Moalin katika benchi la Perdo. Hii haikuwa ishara nzuri kwa Pedro mwenyewe na hapa ina maana Yanga SC walishajiandaa kuishi bila ya yeye.
Kuna usemi wa kiswahili unaosema akipasha kipa hatoki mshambuliaji. Perdo hakuusoma vyema na kuuelewa mstari huu. Kiufupi hakusoma alama za nyakati.
Ingizo la Moalin lilimfanya aanze kutembelea katika uzi mwembamba ambao mpaka kufikia jana jioni umekatika vipande viwili.
Mashabiki hawakuwa na imani nae tangu kipindi kile cha sare mfululizo dhidi ya timu za Mtibwa Sugar, TRA United.
Kuna kikao kizito kilifanyika Jangwani nyakati zile. Kila mmoja aliamini Pedro asingetoboa, kilichotokea tukasikia taarifa ya ujio Moalin.
Tangu siku ile mpaka kufikia jana jioni alichokuwa anakifanya Pedro ni kuendelea kuwaibia muda wao Yanga SC na Yanga SC ni waliutoa wakiamini atabadilika. Hili limeshindikana kutokea. Walichokifanya Yanga SC ni kumbadili yeye. Huwa inatokea katika maisha.
@abdulmkeyenge1





