Amrouche aipeleka Rwanda FIFA
Sisti Herman
March 17, 2026
Share :

Rais wa shirikisho la soka la Rwanda (FERWAFA), Shema Fabrice, amethibitisha kuwa Adel Amrouche, Kocha wa zamani wa Amavubi, amewasilisha malalamiko yake FIFA kwa madai kuwa alifukuzwa kazi kinyume cha sheria.
Januari 2026, FERWAFA ilitangaza kumsimamisha kazi Adel Amrouche kama Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ kwa sababu mbalimbali.
Katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika Jumatatu Machi 16, 2026, Rais wa FERWAFA, Shema Ngoga Fabrice, amethibitisha kuwa Kocha huyo alilishtaki Shirikisho hilo na kwamba pia wako kwenye hatua za kisheria.
Katibu Mkuu wa FERWAFA, Bonnie Mugabe amesema kuwa wana imani malimbikizo ya madeni wanayodaiwa na Kocha wa zamani wa Amavubi yatalipwa hivi karibuni.
Adel Amrouche aliteuliwa kuwa kocha wa Amavubi mnamo Februari 2025, kwa kandarasi ya miaka miwili, na tangu hapo alishinda mechi moja pekee dhidi ya Zimbabwe mnamo Septemba.
Nafasi yake ilichukuliwa na Muingereza Stephen Constantine mwenye umri wa miaka 63, ambaye amepewa kazi ya Amavubi kwa miaka miwili.





