ANC yashutumiwa kutaka kumuua Jacob Zuma
Eric Buyanza
March 30, 2024
Share :
Siku moja baada ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kunusurika katika ajali ya gari, chama chake kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK) kimekishutumu chama tawala cha ANC kwa kuhusika katika ajali hiyo.
Msemaji wa chama cha Zuma cha Umkhonto we Sizwe (MK) Nhlamulo Ndhlela amesema katika taarifa kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, Zuma amenusurika katika ajali mbili zinazowahusisha madereva wanaodaiwa kuwa walevi.
Ndhlela amesisitiza kuwa hili linaonekana kama jaribio la makusudi la kutaka kumuua Zuma ambaye ni mwanasiasa mkongwe na mwenye ushawishi mkubwa.
Msemaji huyo ameongeza kuwa chama hicho "kimekuwa kikifuatilia kwa karibu mlolongo wa matukio yanayoshabihiana" ambayo yamemtokea Zuma chini ya utawala wa "serikali ya Cyril Ramaphosa ", mara tu baada ya Zuma kutangaza mwezi Disemba kwamba atafanya kampeni kwa tiketi ya chama cha MK katika jitihada za kufufua upya safari yake ya kisiasa.
Binti wa Zuma, Duduzile Zuma ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa X (zamani Twitter) na kudai kuwa ajali hiyo ya gari haikuwa bahati mbaya, huku akisisitiza: "Tafadhali msituone wajinga, sisi sio wafuasi wa Ramaphosa".