Askari kuanza kutumia Glovu za umeme kukamata wahamiaji
Eric Buyanza
August 13, 2026
Share :

Maafisa wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha nchini Marekani, ICE, wanaweza kuanza kutumia glovu zinazoweza kutoa mshtuko wa umeme wanapotekeleza majukumu yao ya kiusalama.
ICE imepanga kutumia hadi dola milioni 20 kununua glovu hizo zinazojulikana kama Generated Low Output Voltage Emitter, GLOVE, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Jumatatu na Idara ya Usalama wa Taifa, DHS.
Glovu hizo zina uwezo wa kutoa mshtuko wa umeme wa hadi volti 380, karibu mara tatu ya kiwango cha umeme kinachotolewa na soketi ya kawaida nchini Marekani.
Mashirika ya kutetea haki za kiraia, likiwemo American Civil Liberties Union, ACLU, yameeleza wasiwasi kuhusu matumizi ya glovu hizo.
ICE imekuwa ikikabiliwa na uchunguzi kuhusu mbinu zake wakati wa operesheni za utekelezaji wa sheria, ambazo zimesababisha maafisa wake kuhusishwa katika matukio kadhaa ya watu kuuawa kwa kupigwa risasi.
DHS imeiambia BBC kuwa ICE inaendelea kutathmini mahitaji ya maafisa wake walio katika maeneo ya utekelezaji wa sheria, ili kuhakikisha wanapata vifaa vinavyohitajika kuwakamata na kuwaondoa nchini wahamiaji wanaokiuka sheria za uhamiaji.
Kampuni ya Compliant Technologies LLC, inayotengeneza glovu hizo, imeiambia BBC kuwa haiwezi kutoa maoni kuhusu mauzo hayo.
DHS imesema mkataba wa ununuzi wa glovu hizo bila mchakato wa zabuni unaweza kuchapishwa mapema Ijumaa.
Glovu hizo huwashwa kwa kubonyeza kitufe na zinaweza kutoa hadi mishtuko 30 ya umeme kwa sekunde. Pia zina vichakataji vidogo vinavyorekodi kila matumizi ya kifaa.
Compliant Technologies inasema kwenye tovuti yake kuwa glovu hizo hazisababishi majeraha na zinatumiwa na taasisi mbalimbali za utekelezaji wa sheria.
BBC





