Atandikwa faini kwa kudhihaki kimo cha Waziri mkuu
Eric Buyanza
July 19, 2024
Share :
Mahakama imemuamuru mwanahabari wa kiitaliano Giulia Cortese kumlipa Waziri Mkuu Giorgia Meloni fidia ya Euro 5,000 (sawa na shilingi Milioni 14.5 za kibongo) kutokana na kile alichokichapisha mtandaoni kudhihaki kimo cha waziri mkuu huyo.
Jaji aliamua kwamba machapisho mawili ya mwandishi huyo yalikuwa na nia ya kumchafulia jina Waziri mkuu na yalidhamiria ‘kumuaibisha’.
Akijibu uamuzi huo, Bi Cortese alisema serikali ya Italia ina tatizo kubwa na uhuru wa kujieleza.
Wawili hao waligombana kwa mara ya kwanza Oktoba 2021, baada ya Bi Cortese kuchapisha picha ya dhihaka ya Bi Meloni kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).
Baadaye tena katika chapisho hilo mwandishi huyo aliandika "Hunitishi Giorgia Meloni, kwanza una urefu wa 1.2m tu, Siwezi hata kukuona."
Urefu wa Bi Meloni unaripotiwa katika vyombo vya habari kuwa 1.63m (sawa na 5ft 3in).