Aua mke kwa shoka na kumzika porini, kisa wivu
Eric Buyanza
May 3, 2024
Share :
Mkazi wa kijiji cha Nzigala kata ya Kigwa, Wilayani Uyui Mkoani Tabora Bi.Kaluba Emmanuel (27) ameuawa kwa kukatwa na shoka na mume wake kwa kumtuhumu kuwa ana mahusiano na mwanaume mwingine.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo mnamo Aprili 18 mwaka huu na kubainisha chanzo cha tukio hilo kuwa ni wivu wa kimapenzi baina ya wanandoa hao.
Alisema kuwa ndugu wa marehemu waligundua tukio hilo baada ya kwenda kumtembelea dada yao ambaye hawajamwona muda mrefu na kukuta hayupo ambapo mumewe alidai ametoroka na hajui aliko.
Kamanda Abwao alifafanua kuwa wanafamilia walipotia mashaka na kumuuliza kwanini hakwenda kutoa taarifa polisi juu ya tukio hilo kwa kuwa hajaonekana zaidi ya wiki 2.
Alisema wanafamilia walilazimika kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi ambapo polisi walifika nyumbani hapo na kumchukua mume wa marehemu kwa ajili ya mahojiano ambapo alikiri kufanya mauaji hayo na kuonyesha mahali alipofukia mwili wa mkewe.
Abwao alifafanua kuwa siku ya tukio muuaji alitoka na mke wake kwenda kijiji cha Nzigala “A” na kumtaka waende porini kutafuta Uyoga ndipo akaanza kumshambulia kwa kumkata na shoka sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia kifo.
Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kumuua alichimba shimo na kumfukia katika pori la hifadhi ya Kigwa-Lubuga iliyopo katika tarafa ya Igalula wilaya humo.
Mtuhumiwa huyo ambaye jina limehifadhiwa (30) anashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kumaliza mahojiano na anatarajia kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji.