Auwawa kisa, kucheza muziki na kula juu ya kaburi la mama yake
Eric Buyanza
December 30, 2023
Share :
Huko Kakamega nchini Kenya jamaa mmoja ameuwawa na ndugu zake siku ya mkesha wa Krismasi kwasababu ya kucheza dansi huku akila nyama juu ya kaburi la mama yake.
Inaelezwa kuwa tukio hilo lilijiri baada ya jamaa kurejea nyumbani kwao akitokea mjini kwa ajili ya kusherekea sikukuu ya krismasi na aliamua kumuenzi marehemu mama yake kwa kuimba na kucheza juu ya kaburi lake huku akila nyama.
Sherehe ilibadilika kuwa msiba wake baada ya ndugu zake kukasirishwa na kile walichokiona kwa kudai ni kinyume na utamaduni wao na kuamua kumshambulia na chuma pamoja na mapanga ambapo alivuja damu nyingi kabla ya mauti kumkuta.
Dada wa marehemu, Agnes Anyona, akisimulia kwa machungu kuhusu kisa hicho alisema..."Alikuwa ametoka tu mjini kwenda kuwaona marafiki zake, na alipofika nyumbani, alienda moja kwa moja kwenye kaburi la marehemu mama yetu na kuanza kucheza huku akila nyama....Ndugu zangu wengine wawili waliposikia kuhusu hilo, walikasirika, wakidai kuwa ni kinyume na imani za kitamaduni," alisema Anyona.
Polisi wa Kakamega walithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa mmoja, mwanamume mwenye umri wa miaka 33, na wakatangaza msako unaoendelea wa kumtafuta ndugu mwingine aliyetoroka baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Source: Tuko