pmbet

Aweso amtumbua Mkurugenzi kwa kushindwa kufika Hanang'

Eric Buyanza

December 9, 2023
Share :

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuondoa kwenye nafasi yake Mkurugenzi wa Sehemu ya Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa, Mhandisi Mashaka Sitta baada ya Mhandisi Sitta kutotimiza vema majukumu yake katika eneo hili muhimu la uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa na usimamizi wa mitambo na zaidi kutofika Wilayani Hanang Mkoa wa Manyara baada ya kutokea changamoto ya mafuriko yaliyosababisha vifo 80, majeruhi na uharibifu wa miundombinu ikiwemo ya maji licha ya Maboss zake akiwemo Waziri Aweso kufika Hanang.
 

Kufuatia mabadiliko haya Aweso amemteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa RUWASA Mhandisi Ndele Mengo kuchukua nafasi hiyo ya Sitta na amemuelekeza Mhandisi Ndele kufika mara moja Wilayani Hanang na kuanza kazi ya usimamizi wa uchimbaji wa visima kwa maeneo ambayo miundombinu ya maji imeathiriwa na mafuriko.
 

Aweso amesema mabadiliko haya yamelenga kuimarisha sehemu ya uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa na kusisitiza kuwa mchakato wa uundwaji wa Wakala kamili wa DDCA unaendelea na utakamilika kwa wakati.
 

Katika hatua nyingine Waziri Aweso amemteua Mhandisi Mariam Majala kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ufundi, RUWASA, kabla ya uteuzi huo Majala alikuwa Meneja wa RUWASA mkoa wa Simiyu na amemteua pia Mhandisi Abbas Pyarali kuwa Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Usanifu na Usimamizi wa Miradi ya Maji Wizara ya Maji, awali alikuwa Mhandisi Mkuu katika Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji.
 

Waziri Aweso amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyonayo kupitia Sheria Namba 5 ya Mwaka 2019 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet