Azikwa baada ya siku 579 tangu afariki, mke wake aliamini atafufuka
Eric Buyanza
June 17, 2024
Share :
Mchungaji Siva Moodley wa Afrika Kusini, alifariki Agosti 15, 2021, lakini mwili wake ulizikwa mwezi Machi mwaka huu, baada ya kukaa siku 579 kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, kwa sababu familia yake na waumini wa kanisa lake walikuwa wamkiamini atafufuka.
Kabla ya kifo chake Siva Moodley yeye mwenyewe alikuwa akiamini kwamba watu wanaweza kufufuliwa.
Alifariki baada ya kuugua, hata hivyo katika hali ya kushangaza badala ya kufanya matayarisho ya mazishi familia yake iliuacha mwili huo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti wakingoja afufuke.
Mke pamoja na ndugu wa marehemu walikuwa wakienda kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kumuombea kila wakati ili azinduke, lakini waliacha kwenda mahali hapo kwa miezi kadhaa na walikuwa hawapatikani kila walipotafutwa, jambo lililomlazimu mmiliki wa chumba cha kuhifadhia maiti kulifikisha jambo hilo mahakamani.
Baada ya vuta nikuvute nyingi za kisheria hatimaye Machi 16, 2024, mwili wa Siva Moodley ulizikwa kwenye makaburi ya Westpark jijini Johannesburg, mbele ya ndugu zake na familia yake lakini mke pamoja na watoto wake wawili hawakuhudhuria maziko hayo.