Barcelona kusitisha mechi ya kirafiki Nchini Morocco kisa mgogoro wa uhamiaji.
Joyce Shedrack
July 31, 2026
Share :
Klabu ya Barcelona inafuatilia kwa karibu hali ya mgogoro wa uhamiaji unaoendelea kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya nchini Morocco katika jiji la Tangier, iliyopangwa kufanyika Jumamosi, Agosti 15.

Kwa mujibu wa gazeti la Hispania Mundo Deportivo, Barcelona tayari imekamilisha makubaliano na waandaaji wa Morocco kuhusu mchezo huo. Hata hivyo, tangazo rasmi la mechi hiyo limesitishwa kutokana na mgogoro wa uhamiaji uliosababishwa na maelfu ya raia wa Morocco kuingia katika mji wa Ceuta.
Ripoti zinaeleza kuwa picha za hali ilivyo katika mpaka wa Ceuta zimeifanya Barcelona kutafakari upya kuhusu mchezo huo. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Hispania, takribani watu 49,000 waliingia Ceuta kwa kuogelea baharini, idadi inayozidi nusu ya wakazi wa mji huo wenye jumla ya watu 84,208. Aidha, watu wasiopungua 18 walipoteza maisha katika tukio hilo.
Barcelona inasubiri kuona maendeleo ya hali hiyo na haijaondoa uwezekano wa kujiondoa kwenye mchezo huo dhidi ya timu ambayo haijawekwa wazi jina lake ikiwa mgogoro utaendelea kuwa mbaya zaidi. Hata hivyo, mechi hiyo ilikuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya kocha Hansi Flick kuelekea mchezo wa kwanza wa La Liga dhidi ya Elche, uliopangwa kuchezwa Agosti 23.
Iwapo mechi ya Morocco itafutwa, Barcelona itabaki na mchezo mmoja tu wa maandalizi, ambao ni Kombe la Joan Gamper dhidi ya Al Ahly ya Misri, utakaochezwa Agosti 19 katika uwanja wa Spotify Camp Nou.





