Barnaba na wenzake kizimbani kwa kutuma SMS za 'Jiunge na Freemason'
Eric Buyanza
May 29, 2024
Share :
Mahakama ya ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapandisha kizimbani wakazi wa Ifakara, Morogoro akiwemo Barnaba Gidajuri na wenzake 11 wakikabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia pesa shilingi millioni 10 kwa njia ya udanganyifu.
Wakiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Mhe. Ushindi Swalo, Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru alidai kuwa watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka 32.
Wakili Mafuru alidai mashtaka hayo ni kuongoza genge la uhalifu waliofanya Januari mosi hadi Mei 5, 2024, ambapo walituma jumbe fupi kwa watu kisha kujipatia kiasi cha Sh millioni 10.
Aidha, Wakili Mafuru alidai kuwa shtaka la pili na la tatu yanayomkabili mtuhumiwa Barnaba Gidajuri ilitotenda Januari 4, 2024, la kusambaza jumbe fupi kwa njia ya mtandao wenye maneno "Mzee huyu Mganga wa tiba asili anatoa mali bila kafara, cheo, mapenzi......", "jiunge na chama huru cha freemason (666) Tanzania bila kutoa kafara ya binadamu.....".
Kwa mujibu wa Wakili mashtaka mengine manne yanayomkabili Barnaba ni pamoja na alipokuwa mkoani Morogoro alitumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina tofauti bila ruhusa.
Aliendelea kwa kudai kuwa shtaka la nane linalomkabili mtuhumiwa huyo alilitenda Mei 11, 2024 kwa kujipatia shilingi 105,000 kutoka kwa Maria Nangwa baada ya kujitambulisha kuwa ni Mganga atakayemtibia ugonjwa wake wa kifafa.
Mahakamani hapo Wakili alidai mashtaka tisa na kumi yanayomkabili mtuhumiwa Rahim Bangila (26), kwa kusambaza jumbe fupi kwa njia ya mtandao wenye maneno."Mimi mwenye nyumba wako apa mbona siku zinazidi?"
Wakili Mafuru alidai mtuhumiwa Rahim anakabiliwa ni mashtaka matatu kwa kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya Valence Mandaki, Nundu Gulenya na Stephen Lihami bila ruhusa ya watu hao.
Aidha, Wakili alidai mtuhumiwa mwingine Ramadhan Mcheni (28) anakabiliwa na mashtaka mengine mawili ya kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine bila ruhusa yao.