Bashungwa amuondoa Mhandisi mshauri, aagiza Mkandarasi kutopewa miradi mingine
Eric Buyanza
January 25, 2024
Share :
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa Mhandisi Mshauri LEA Associaties anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kitai - Lituhi sehemu ya Amani Makoro-Ruanda (km 35) kwa kiwango cha lami na kuutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuendelea kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika.
Pia, ameagiza Mkandarasi anayejenga barabara hiyo China Railway Seventh Group kutopewa miradi mipya mpaka hapo atakapokamilisha miradi aliyopewa katika mkoa wa Mara, Katavi ambayo nayo inaonekana kusuasua.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo tarehe 25 Januari 2024 wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo ambapo hajaridhishwa na utekelezaji wake ambao umechelewa kwa asilimia 75 na kusisitiza hatua za kimkataba zichukuliwe dhidi ya Mhandisi Mshauri huyo.
“Nimuagize Katibu Mkuu kuangalia hatua za kimkataba mnazotakiwa kumchukulia haraka Mhandisi Mshauri kwasababu ameshindwa kumsimamia Mkandarasi kukamilisha mradi huu kwa wakati”,amesisitiza Waziri Bashungwa.
Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishatoa Bilioni 6.9 ambayo imekamilisha kipande cha kwanza cha kilometa 5 kutoka Kitai hadi Amani Makoro na Bilioni 60 kwa ajili ya muendelezo wa barabara hiyo sehemu ya Amani Makoro - Ruanda.
“Kiasi cha Shilingi Bilioni 155 zimetengwa ajili ya mradi mzima wa ujenzi wa barabara kuanzia Kitai - Lihuli - Bandari ya Ndumbi”, amefafanua Bashungwa.
Bashungwa ameagiza TANROADS kutoendelea kulimbikiza miradi kwa Wakandarasi kwani ndiyo inafanya miradi mingi kuchelewa na mingine ikiwa ya kimkakati na kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, amesema kuwa maendeleo ya mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 100 ambapo mradi huo ulitakiwa kukamilika Disemba, 2023.