Bellingham akubali mkataba mpya Real Madrid hadi mwaka 2031
Eric Buyanza
October 17, 2026
Share :

Kiungo mahiri wa kimataifa wa Uingereza, Jude Bellingham, amefikia makubaliano ya mkataba mpya wa muda mrefu na klabu ya Real Madrid, hatua inayozika rasmi uvumi wa tetesi za yeye kurejea kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mkataba wa sasa wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ulikuwa unamalizika mwaka 2029. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti kutoka nchini Hispania na mwandishi wa habari za michezo Fabrizio Romano, makubaliano hayo mapya yanamfunga Bellingham katika dimba la Santiago Bernabeu hadi tarehe 30 Juni 2031.
Mbali na kuongeza muda wa miaka miwili zaidi, mkataba huo mpya unakuja na ongezeko kubwa la mshahara linaloakisi mchango wake mkubwa na nafasi yake kama mmoja wa viongozi wapya ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha Real Madrid.
Ripoti za ndani zinaashiria kuwa maslahi yake mapya yanaweza kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji wa Kiingereza wanaolipwa pesa nyingi zaidi duniani.





