Benchikha amsamehe Chama, amwita Kigoma haraka
Sisti Herman
February 2, 2024
Share :
Baada ya uongozi wa Klabu ya Simba kutangaza msamaha kwa kiungo Mzambia, Clatous Chama ambaye aliadhibiwa Desemba 21, 2023 kutokana na utovu wa nidhamu, meneja habari na mawasiliano wa timu hiyo Ahmed Ally amechapisha picha kwenye mtandao wake wa kijamii akiwa na Chama kuelekea Kigoma kujiunga na timu hiyo inayojiandaa na mchezo wa ligi dhidi Mashujaa Fc ya mkoani humo.
Taarifa ya msamaha huo ilitolewa leo na Afisa Mtendaji Mkuu, Imani Kajula ikieleza kumsamehe mchezaji huyo baada ya kuwa nje kwa siku 40.
Katika taarifa hiyo uongozi wa Simba umesema “Hatua hii imetokana na maamuzi ya kamati ya ufundi ya Bodi ya Simba ambayo ilipitia barua ya maelezo ya Chama na uamuzi wa Kocha Benchikha wa kumsamehe kiungo huyo, hivyo kamati ya ufundi ya bodi ya hiyo ikaridhia kumsamehe na kusitisha kumfikisha kwenye kamati ya maadili ya klabu hiyo.”
“Chama anaungana na kikosi cha Simba kilicho mkoani Kigoma kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho Februari 3 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
“Klabu ya Simba itaendelea kutilia mkazo ustawi wa nidhamu kama nguzo muhimu ya kujenga timu imara. Nidhamu ni moja ya tunu za klabu ya Simba.”