Benchikha awakusanya mastaa Simba haraka
Joyce Shedrack
January 26, 2024
Share :
Baada ya kumalizika kwa likizo fupi ya siku 10 iliyotolewa na benchi la ufundi chini ya kocha Mualgeria Abdelhak Benchikha kwa wachezaji wa klabu hiyo baada ya mchezo wa fainali uliopigwa kule visiwani Zanzibar na Simba sc kupoteza fainali hiyo, klabu ya Simba sc imetoa taarifa kwa wachezaji wake wote ambao hawako kwenye michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (AFCON 2023) kurejea haraka kambini kwa ajili ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi zijazo za ligi, maandalizi yatakayofanyika kwenye uwanja wao wa mazoezi wa Mo Simba Arena, Bunju jijini Dar es salaam.
Benchi la ufundi la Simba SC lilitoa programu maalumu ya mazoezi kwa kila mchezaji atakayokuwa anafanya akiwa nyumbani kwake ili kutopoteza utimamu wa mwili wakati huu ambapo ligi kuu ya Soka Tanzania bara imesimama kupisha michuano ya Mataifa ya Afrika Afcon 2023 yanayoendelea nchini Ivory Coast.
Katika michuano hiyo Simba SC ilikuwa na wachezaji sita walioitwa kuziwakilisha timu zao za Taifa kwenye mashindano ya Afcon 2023 wazawa wa nne Aishi Manula, Mzamiru Yassin, Kibu Denis na Mohamed Hussein huku wachezaji wa kigeni wakiwa ni wawili pekee ambao ni Henock Inonga (DR Congo), na Clatous Chama (Zambia), Mchezaji pekee wa Simba ambaye timu yake bado ipo kwenye michuano hiyo ni Henock Inonga ambaye timu yake ya Taifa imefanikiwa kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.
“Tunarudi kwenye raha binafsi siyo za ku share leo january 25 mnyama anarudi rasmi kwenye uwanja wa mazoezi kujiandaa na mashindano yaliyo mbele yetu likizo imekwisha tunarudi kazini ” alinukuliwa Ahmed Ali, meneja wa idara ya habari na mawasiliano wa kla bu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Simba baada ya mapumziko hayo, itatupa karata yake ya kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, Februari 17, mwaka huu dhidi ya Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo kwa mujibu wa ratiba ya bodi ya ligi kuu Tanzania bara (TPLB).