Benki yapunguza wafanyakazi 5000 ili kutumia AI
Sisti Herman
October 22, 2026
Share :

Benki ya Barclays Group imetangaza kupunguza takribani ajira 5,000 huku ikieleza mbadala wake ni kutumia akiliunde zaidi katika shughuli zake.
Taarifa iliyochapisha leo Alhamisi Oktoba 22, 2026 na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Mtendaji Mkuu wa Benki ya Barclays Group, Coimbatore Venkatakrishnan amesema upunguzaji wa ajira umetokana na uwekezaji mkubwa ambao benki hiyo inaufanya katika teknolojia kwa lengo la kurahisisha na kuboresha shughuli zake za kibiashara.
Amesema Barclays Group imesema nafasi za kazi 1,000 tayari zimeondolewa na inatarajia kukamilisha upunguzaji wa nafasi nyingine 4,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Upunguzaji huo unahusisha asilimia tano ya wafanyakazi wake duniani kote, huku nafasi nyingi zikihusisha shughuli za uendeshaji na majukumu ya kiutendaji. Barclays imesema hatua hiyo imetokana na uwekezaji katika teknolojia, ambapo akiliunde inasaidia kufanya baadhi ya michakato ya kazi kuwa na ufanisi zaidi.
Wanauchumi wamekuwa wakifuatilia kwa makini matokeo ya kampuni mbalimbali ili kubaini iwapo uwekezaji katika teknolojia mpya, hususan akiliunde, unaanza kuleta mabadiliko katika shughuli zao za kila siku kwa kuongeza ufanisi na kupunguza ajira.





