Bibi aukana uraia wa Marekani, asema anataka kufia India
Eric Buyanza
June 30, 2026
Share :

Bibi mwenye umri wa miaka 94 aliyefahamika kwa jina la Kondragunta Mahalakshmamma ametikisa mitandao ya kijamii mwezi huu baada ya kutangaza kuukana uraia wake wa Marekani kwa sababu ana hamu kubwa ya "kufa akiwa Mhindi" katika ardhi ya nyumbani kwao India.
IKO HIVI
Baada ya kifo cha mume wake, Bibi huyu alihamia Marekani na kuishi na mtoto wake wa kiume, Dkt. Buchaiah Choudhary, ambaye ni daktari wa magonjwa ya saratani huko kwenye jimbo la Virginia nchini Marekani.
Alifanikiwa kupata uraia wa Marekani mnamo Julai mwaka 2000 na kuishi huko kwa takriban miaka 18.
Mwaka 2018 mtoto wake aliamua kurudi India kufanya kazi katika Hospitali za huko, bibi Mahalakshmamma alichagua kurejea na mwanae na kuhamia kijijini kwao Chinthagumpala. Hata hivyo, kwa kuwa sheria za India haziruhusu uraia pacha (dual citizenship), ilimlazimu kuchagua nchi moja.
Akiwa anakaribia umri wa miaka 95, alifanya maamuzi ya kuachana rasmi na pasipoti ya Marekani na kuomba kurejeshewa uraia wake wa India.
Video ya bibi huyu ilisambaa mitandaoni ikimwonyesha akifika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bapatla kuchukua kiapo cha uaminifu kwa Katiba ya India.
Alisema maneno haya ya kugusa hisia:
“Mkuu wangu, nakaribia miaka 95 sasa. Nia yangu pekee ni kutumia siku zangu za mwisho katika nchi yangu ya kuzaliwa kama raia wa India. Nataka maziko yangu yafanyike kwenye kijiji changu cha asili.”





