Binti msajili laini alawitiwa na vijana wanne Arusha.
Joyce Shedrack
October 6, 2026
Share :
Binti mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya kulinda faragha yake, amedai kubakwa na kulawitiwa na vijana wanne katika Mtaa wa Sanare, Kata ya Daraja Mbili, jijini Arusha.
Akisimulia tukio hilo, binti huyo amesema kazi yake ni kusajili laini za simu na siku hiyo alikuwa akipita mitaani kutoa huduma hiyo.
Amesema akiwa katika shughuli zake, alikutana na kijana mmoja aliyemweleza kuwa anahitaji kusajili laini ya simu, lakini akamwomba aende nyumbani kwake kwa sababu mke wake alikuwa mzazi na hakuwa na uwezo wa kutoka nje.
Kwa mujibu wa maelezo yake, alipofika nyumbani hapo na kuingia ndani, kijana huyo alifunga mlango, kisha akatoa kisu na kumtaka avue nguo zote.
Binti huyo amesema kijana huyo alianza kumfanyia ukatili wa kingono kwa nguvu, kabla ya vijana wengine kufika na kuungana naye, ambapo anadai jumla yao walikuwa wanne na wote walimfanyia vitendo hivyo.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kufika mara moja katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo.
Tukio hilo linadaiwa kuwa la ukatili mkubwa, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa kwa mujibu wa sheria.





