Binti wa miaka 16 mbaroni akituhumiwa kuiba mtoto
Eric Buyanza
July 22, 2024
Share :
Binti aliyefahamika kwa jina la Maduki Sabuni, mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Imalanguzo Ushirombo Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuiba mtoto wa miezi 9, aliyemuiba wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amebainisha hayo leo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Amesema Julai 18 mwaka huu, katika Stendi ya mabasi Manzese wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kulitokea tukio la mtoto kuibiwa aliyefahamika kwa jina la Meresiana Paschal miezi 9 wakati mama yake akiendelea na shughuli za utafutaji riziki kwenye stendi hiyo, ambapo mtu aliyemuimba alikimbia naye kusikojulikana.
Amesema Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa za wizi wa mtoto huyo, alilianza kufanya upelelezi na kwamba Julai 21 mwaka huu, huko maeneo ya Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita na kufanikiwa kumkamata binti Maduki Sabuni (16) akiwa na mtoto huyo.
“Polisi tulifanya mahojiano ya awali na binti huyu, na amekiri kutenda kosa la kuiba mtoto huyo, na bado tunaendelea kumhoji zaidi,”amesema Magomi.
Amesema mtoto huyo amepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya kabla ya kumkabidhi kwa mama yake mzazi.
Ametia wito pia kwa wazazi mkoani Shinyanga, kwamba wawe na uangalizi wa karibu kwa watoto wao,na siyo kuwaacha hovyo hovyo.
Aidha,Kamanda amekemea vikali na kutoa onyo kwa mtu au watu ambao wamekuwa wakihusika na vitendo vya wizi wa watoto, sababu katika Mkoa wa Shinyanga tukio la namna hiyo ni la pili kutokea, na kwamba hatua kali za kesheria zitachukuliwa dhidi ya watu watakaondelea kuhusika na matukio hayo.