Biteko aagiza bodi ya ETDCO kuvunjwa, kisa wizi na utendaji mbovu
Eric Buyanza
March 28, 2024
Share :
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuvunjwa kwa Bodi ya Kampuni Tanzu ya TANESCO ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) na kuundwa upya kwa Menejimenti ya Kampuni hiyo kutokana na utendaji kazi mbovu, wizi fedha za umma ndani ya Shirika pamoja na wizi wa vifaa vya umeme uliokithiri.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa Kikao kazi baina yake na Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni zake tanzu, Wakurugenzi wa TANESCO wa Kanda na Mameneja wa Mikoa ambacho kimefanyika tarehe 28 Machi, 2024 jijini Mwanza kikiwa na lengo la kujadili utendaji kazi katika Sekta ya umeme.
Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya TANESCO kuagizwa kumuondoa Meneja Mkuu wa ETDCO kutokana na utendaji mbovu wa kazi ndani ya Taasisi na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya umeme ukiwemo wa usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Urambo na Tabora hadi Mpanda.
Maamuzi hayo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, yametokana baadhi ya watendaji wa TANESCO na kampuni zake Tanzu kushindwa kutekeleza maelekezo yake aliyoyatoa tarehe 2 Desemba 2023 ya kupambana na rushwa, kujenga mahusiano na wananchi wanaowahudumia, kuimarisha uaminifu ndani na nje ya Taasisi, kuacha visingizio na kutatua matatizo ya umeme yanaapojitokeza.
Dkt. Biteko ameagiza Watumishi wote wanaojihusisha na wizi ndani ya Shirika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwaweka pembeni katika Utumishi maana wao ni sababu ya watanzania kutokupata umeme wa uhakika.
Aidha ameelekeza wananchi waliotoa taarifa zilizopelekea kubaini wezi hao wa vifaa vya umeme kupewa barua za pongezi na fedha taslimu.
Dkt. Biteko amewataja baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa TANESCO ambao wamekuwa wakishiriki kufanya wizi wa vifaa mbalimbali ikiwemo vyenye asili ya shaba, mafuta ya transfoma, vifaa vya miradi na ujenzi wa laini haramu ambazo hazipo kwenye mipango ya TANESCO huku mtumishi akiwa amelipwa pesa binafsi.