Biteko azindua Zahanati Ilala
Eric Buyanza
December 29, 2023
Share :
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko leo tarehe 29 Disemba, 2023 amezindua Zahanati ya Bungoni iliyopo mtaa wa Mafuriko Ilala jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi kutumia zahanati hiyo badala ya kwenda mbali kwani ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.
"Niwaombe viongozi wenzangu tuliopewa dhamana na Rais kuhakikisha tunawahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge kwa kuwapatia huduma bora wanazostahili." Amesisitiza Dk. Biteko.
Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwezi februari mwaka huu, kwa jitihada za wananchi na baadae Serikali na umegharimu kiasi cha shilingi milioni 351, ukihusisha gharama za ujenzi, samani, dawa na vifaa tiba na umefadhiliwa na African Relief Agency na Taasisi ya Rahma International kutoka Kuwait na inamilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali.
Zahanati hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia kata nne zilizopo wilaya ya Ilala ambazo ni Ilala, Buguruni, Sharifu Shamba, na Mchikichini wapatao Elfu 12.