Bondia Zolani Tete apigwa risasi na kuuawa nje ya nyumba yake
Eric Buyanza
August 22, 2026
Share :

Bingwa wa zamani wa dunia wa bondia, Zolani “Last Born” Tete amepigwa risasi na kuuawa nje ya nyumba yake katika mkoa wa Eastern Cape nchini Afrika Kusini hapo jana, polisi na Waziri wa Michezo wa nchi hiyo wametoa taarifa.
Tete, mwenye umri wa miaka 38, alikuwa akielekea nyumbani kwake katika mji wa Mdantsane wakati wanaume wawili waliokuwa na silaha na waliovaa barakoa waliposhuka kutoka kwenye gari na kuanza kumfyatulia risasi.
Kuuawa kwa Tete kunaamsha tena mjadala kuhusu uhalifu wa kimabavu Afrika Kusini. Taifa hilo linaendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani licha ya kupungua kwa idadi ya mauaji katika kipindi cha hivi karibuni.
Kifo cha bingwa huyo wa bondia duniani pia kimewagusa sana wakazi wa Mdantsane, mji wa Eastern Cape, mji ambao umezalisha baadhi ya mabondia waliofanikiwa zaidi nchini Afrika Kusini.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 27 aliyekuwa akisafiri pamoja na Tete alipigwa risasi mara kadhaa na kukimbizwa hospitalini.
Polisi wameanza uchunguzi, huku chanzo na sababu ya bondia huyo kushambuliwa bado haijajulikani.
Tete alitwaa taji la dunia la IBF katika uzani wa junior-bantamweight mwaka 2014 baada ya kumshinda Mjapani Teiru Kinoshita mjini Kobe, Japan. Baadaye alitwaa pia taji la WBO katika uzani wa bantamweight.
Kimataifa, Tete anakumbukwa zaidi kwa kumpiga ndani ya sekunde 11 raia mwenzake wa Afrika Kusini, Siboniso Gonya, mjini Belfast, Ireland Kaskazini, mwezi Novemba 2017.
Ushindi huo uliweka rekodi ya kumalizika kwa haraka zaidi pambano la kuwania taji la dunia.





