Boti ya Kisasa kurahisisha uokozi na matibabu ukanda wa Ziwa.
Joyce Shedrack
July 7, 2025
Share :
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo julai 07, 2025 amekagua Meli ya Kisasa ya Uokozi na Matibabu iliyojengwa kwa gharama ya Tshs. Bilioni 4.5 chini ya mradi wa Kikanda wa Usafiri na Mawasiliano Ziwa Victoria unaojumuisha nchi ya Tanzania na Uganda.
Akizungumza wakati wa majaribio kutoka bandari ya Mwanza Kaskazini na kurudi Mkuu wa Mkoa ameishukuru serikali ya awamu wa sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye eneo la ziwa victoria ili kuhakikisha wananchi wake wanakua salama wanaposafiri na kufanya shughuli za uvuvi.
“Tunashukuru Serikali ya awamu ya sita kwa utekelezaji wa mradi huu ambao unakaribia kukamilika”.
Na moja ya mambo yaliyo chini ya mradi huu ni pamoja na kuweka mawasiliano na kujenga kituo cha Kikanda cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji kilichopo Ilemela na ununuzi wa boti hii pamoja na boti mbili ndogo za utafutaji na uokoaji. Amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, amesema boti hiyo ya kisasa italeta fursa kwa wagonjwa watakaopata dharula zozote ndani ya maji, boti hiyo itawafikia kwa haraka na kutoa Matibabu ya dharura kabla ya kufikishwa nchi kavu kwa ajili ya kupelekwa hospitali ya rufaa katika eneo husika.
Naye Afisa Mfawidhi Mkoa wa Mwanza kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Joseph Mkumbo amesema boti hiyo ya kisasa ina uwezo wa kutembea maili 18 kwa saa.
Aidha, amebainisha kuwa imewasili mkoani Mwanza kutoka bandari ya Mtwara tarehe 23 Juni, 2025 na kwamba kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza walifanikisha kuishusha majini tarehe 05 Julai 2025 kwenye bandari ya Mwanza Kusini.
Ameongeza kuwa tayari TASAC wameifanyia majaribio majini na kuonesha mafanikio makubwa sana kwani imetumia muda wa saa 1 kwenda Ukerewe tofauti na meli zinazotumia masaa 3 hadi 4 na ameongeza kuwa mradi huo unahusisha pia ununuzi wa boti mbili zingine zenye vifaa.