pmbet

Bubista alivyoifanya Cape Verde kuacha alama Kombe la dunia 2026

Sisti Herman

July 15, 2026
Share :

Utangulizi 

Baada ya mchezo wa hatua ya 32 bora ya kombe la dunia 2026 dhidi ya Cape Verde, kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Argentina Lionel Scaloni alinukuliwa akisema maneno haya;

 

 

Maneno hayo ya Scaloni hayakuja tu hivihivi, bali ni kwasababu ya ushindani wa kimbinu ambao Argentina iliupata kutoka kwa Cape Verde chini ya kocha Pedro Leitão Brito ‘Bubista’.

 

Licha ya kupoteza 3-2, Cape Verde walionyesha nidhamu kubwa ya kimbinu dhidi ya Argentina kama walivyofanya kwenye mechi zingine 3 za hatua ya makundi, utofauti baina yao na wapinzani wao ulikuwa ubora wa wachezaji kiufundi, kiakili na utimamu wa kimwili Kama;

 

1. Hispania, nafasi ya 2 kwa ubora duniani
2. Uruguay, nafasi ya 16 kwa ubora duniani
3. Saudi Arabia, nafasi ya 61 kwa ubora duniani
4. Argentina, nafasi ya kwanza kwa ubora duniani

 

Mbinu za Bubista zilizowabeba Cape Verde.

 

Nidhamu kubwa ya Cape Verde kimbinu ilionekana kwa namna timu hiyo inavyowasilisha mbinu zake uwanjani kwa mifumo/miundo ya uchezaji, staili za uchezaji kwenye nyakati zote za kimbinu uwanjani dhidi ya wapinzani wao, nyakati hizo ni;

 

Timu isipokuwa na umiliki wa mpira (Out Of Possession)

 

Kutokana na aina ya wapinzani waliokutana nao, ilitegemewa kuwa kwenye kila mchezo watakaoingia uwanjani, Cape Verde wangepaswa kutawala zaidi mchezo kwa kuzuia zaidi nyakati nyingi ili kumeza ubora wa kiufundi wachezaji wa wapinzani wao. 

 

Cape Verde walifanya hivyo kwa ufanisi wa kiwango cha juu kwani kwa wastani kwenye mechi zote 4 za kombe la dunia waliweza kuwa na umiliki wa mpira wa 33.2% huku nyakati nyingi wakizuia nyuma ya mpira hasa kwenye theluthi zao mbili za nyuma (Mid & Low Block) lengo likiwa ni kuzuia njia za wapinzani wao kweza kuwafikia kirahisi na kuwadhuru. 


 

Kwenye mechi zote hizo Cape Verde walizuia zaidi na mfumo wa 4-1-4-1 ambao ulinyumbulika kwenye miundo tofuati kulingana na theluthi ambapo wapinzani wanamiliki mpira;

 

• 4-1-4-1 - Mpira ukiwa kwenye theluthi ya mbele (High Block)

 

Cape Verde walizuia kwa shinikizo la chini wakizuia njia za wapinzani wao kuweza kujenga shambulizi kuanzia nyuma  (buid up from back) na kuzuia wachezaji wa timu pinzani kuendeleza kirahisi (build up progression) ambapo;

 

 - Mstari wao wa mbele ulikuwa na mchezaji mmoja, Livramento (Tavares/Da Costa) ambaye mara nyingi huwa dhidi ya wachezaji watatu wa timu pinzani, kipa na mabeki wa kati

 

- Mstari unaofuata huwa na wachezaji wanne, viungo washambuliaji wawili wa kati Monteiro na Duarte (J. Duarte/ D. Duarte au Arcanjo) dhidi ya viungo wawili wa kati wa timu pinzani, na pembeni viungo washambuliaji wa pembeni Mendes na J. Carbal dhidi ya mabeki wa pembeni wa timu pinzani

 

- Nyuma ya hao viungo washambuliaji wanne anasimama kiungo wao wa kati Lenin mbele ya mabeki kuzuia kiungo mshambuliaji wa timu pinzani kupokea mipira na kuwachezesha washambuliaji wake

 

• 4-5-1 - Mpira ukiwa kwenye theluthi ya kati na nyuma (Mid & Low Block)
 

Cape Verde walizuia kwa shinikizo la chini na kuwaachia mpira wapinzani wao huku wao wakizuia njia za wapinzani wao kuweza kupenya mistari yao mitatu ya uzuiaji na kuweza kuwafikia kirahisi, njia hizo ni;

 

 - Njia ya kati (Central penetration & creation of chances) ambapo kwenye Mstari wao wa kwanza wa uzuiaji mshambuliaji mmoja, Livramento (Tavares/Da Costa) alisimama kuzuia njia za mabeki wa timu pinzani kupenyeza pasi kwa viungo wao, huku nyuma yake kukiwa na viungo watano, wale viungo washambuliaji wawili wa kati Monteiro na Duarte (J. Duarte/ D. Duarte au Arcanjo)  waliokuwa usawa wa kiungo wa kati Lenin kuzuia njia ya viungo wa timu pinzani kucheza na washambuliaji wao.

 

- Njia ya pembeni, Mendes na J. Carbal walikuwa sambamba na viungo watatu wa kati kwenye mstari wa watu watano nyuma ya mshambuliaji mmoja, lengo likiwa ni kuzuia wachezaji wa pembeni kutoweza kuwazidi idadi mabeki wao wa pembeni, L. Carbal na Moreira kwenye channel za pembeni hasa pale mabeki wa pembeni wa timu pinzani wanaposogea kuongeza idadi kwenye theluthi ya mwisho.

 

- Njia ya juu, baada ya kuzuia vizuri njia ya kati na ya pembeni, wapinzani wao walilazimika kupita njia za juu, huko nako mabeki wao wa kati Pico na Diney walijitahidi kujaribu kushinda mipira ya juu na ya pili japo mara kadhaa walizidiwa ubora na kuadhibiwa

 

• 6-3-1 Theluthi ya chini (Low Block) 

 

Kwasababu wapinzani wao walipenda kucheza zaidi kwa njia za pembeni, Cape Verde pia walizuia kwa ubora mkubwa channel za pembeni kwa kuunyumbulisha muundo wao wa 4-5-1 na kuwa 6-3-1 ambapo mabeki wao wa pembeni wakizuia ndani zaidi karibu na mabeki wa kati, viungo washambuliaji wa pembeni Mendes na J. Carbal walisogea usawa wao na kutengeneza idadi ya watu 6 kwenye mstari wa mwisho.

Licha ya kuwa ni timu iliyokuwa ikizuia vizuri pia kuna nyakati walizidiwa ubora na hapo ndipo utakapotaja uwezo wa wachezaji binafsi kuamua matokeo hasa kipa wao Vozinha ambaye aliibuka shujaa kwenye michezo yao karibu yote akiwa na jumla ya saves (mipira ya kuokoa) 18 huku akifanya saves 7 dhidi ya Hispania na zingine 8 dhidi ya Argentina.

 

Timu ikipora umiliki wa mpira (Offensive Transition)

 

Hii ilikuwa njia bora ya Cape Verde kufanya mashambulizi ya kujibu dhidi ya wapinzani wao ambapo walijaribu kufanya mashambulizi ya kujibu kwa haraka pindi wanapopora mpira kabla ya wapinzani wao kurejea kwenye muundo mzuri wa kuzuia (Counter attacks).

 

Kati ya magoli manne waliyofunga Cape Verde, goli 2 zimetokana na moment hii, mfano wa goli walilofunga kwa wakati kama huo ni goli la pili la kusawazisha dhidi ya Uruguay ambapo walizuia kwa shinikizo kubwa mpira ukiwa kwenye theluthi ya kati ya uwanja na kujibu shambulizi kwa kushambulia nafasi kubwa iliyokuwa baina ya mtu na mtu, mstari na mstari hali iliyosababisha kipa wa Uruguay kutoka golini ili kuwazibia walinzi wake makosa lakini akashindwa pia kuziba kosa hilo hadi alipoadhibiwa na mshambuliaji wa Cape Verde Helio Varela aliyeangia kipindi cha pili.
 

 

Lakini pia ukiachilia mbali goli hilo, Cape Verde wamekuwa na nyakati nyingi bora za kujibu mashambulizi kila wanapopora mpira ambapo kwenye mechi zote nne walizocheza wamefanya jumla ya mashinikizo (Pressing Applied) 1252 wachezaji wa timu pinzani kukosea wakiwa na mpira huku kati ya hayo wakifanya jumla mashambulizi ya kujibu 191 (forced turn overs) huku mawili yakizaa magoli

 

Silaha yao kubwa ni Kasi wa wachezaji (mfano kama Laros Duarte aliyekuwa na mwendokasi wa 6.95 km/h na Ryan Mendes aliyekimbia kwa kasi Mara 170, lakini pia wachezaji kuweza kukimbia umbali mrefu mfano Diney Borges aliyekimbia jumla ya 43.34 km.

 

Timu ikiwa na umiliki wa mpira (In Possession)

 

Kwa aina ya wapinzani iliokutana nao, Cape Verde haikuwa timu yenye uwezo wa kumiliki mpira kwa muda mrefu ambapo kwenye jumla ya mechi zote imekuwa na wastani wa umiliki wa mpira wa 37% tu huku kwenye mchezo mgumu kuliko yote waliyocheza, dhidi ya Hispania wakirekodi umiliki wa mpira wa 26% tu.

 

Licha ya kuwa timu isiyokuwa na umilki wa mpira muda mrefu, mara chache ilizokuwa nao walikuwa timu inayocheza kwa mkakati wa kucheza pasi fupi kutokea nyuma lengo likiwa ni kukaribisha presha ya wapinzani wao ili wapate nafasi ya kuweza kupita katikati ya mistari ya uzuiaji ya wapinzani au nyuma, wakiwa na muundo wa 3-3-4-1, ambapo;

 

 

- Mstari wao wa kwanza wa ujenzi wa shambulizi uliundwa na Kipa wao Vozinha na mabeki wawili wa kati, Diney na Pico ambao mpira ulianzia kwao ili kuvuta presha ya wapinzani (Build up from back)

- Mstari wao wa pili uendelezaji wa shambulizi ulikuwa na kiungo mmoja wa kati, Lenin aliyekuwa akipokea mipira nyuma ya mstari wa kwanza wa uzuiaji wa timu pinzani kwaajili ya kuendeleza shambulizi kwa njia ya kati (Central Build up progression) na mabeki wawili wa pembeni, Moreira na Lopes Cabral kwaajili ya kuendeleza shambulizi kwa njia ya pembeni (Wide Build up progression)

 

Silaha yao kubwa ikiwa ni kipa wao Vozinha alikuwa na uwezo mzuri wa kiufundi kujenga mashambulizi kuanzia nyuma ambapo ambapo amepiga jumla ya pasi 106 zinazovunja mistari huku beki wake Pico akipiga pasi nyingi zilizokamilika zinazovunja mistari, 68 bila kumsahah mwenzake Diney aliyeongoza kwa jumla ya pasi nyingi uwanjani.

 

Wakiwa kwenye nusu ya wapinzani anayezuia kwa Low & Mid Block, muundo wao wa uchezaji ulibadilika na kuwa 2-4-4 ambapo;

 

 

- Watu wawili wa nyuma ni Mabeki wa kati, Diney na Lopes huwa kwenye mstari wa nyuma
- Watu wanne wa kati ni; Lenin na Laros Duarte kama viungo wa kati na pembeni mabeki wawili wa pembeni Moreira na Lopes Cabral wakiwa pembeni yao
- Watu wanne wa mbele wakiwa mshambuliaji wa kati, Livramento na kiungo mshambuliaji wa kati Monteiro na pembeni Mendes na J. Cabral.

 

Wakiwa kwenye theluthi hii wanatumia zaidi ushirikiano wa wachezaji wa pembeni kwa pasi fupi ili kuweza kupenya kuta za uzuiaji za wapinzani na kufika kwenye eneo la mwisho (Sideways combination) ambapo wanatengeneza pembetatu muhimu pembeni mwa uwanja kati ya mabeki wa pembeni kwenye mapana ya uwanja (flanks)  viungo washambuliaji wa pembeni kwenye Channel za ndani (Half space) huku zikiunganishwa na viungo Lenin na Laros Duarte.

 

Kuna wakati wakiwa kwenye theluthi ya mwisho huwa kwenye muundo wa 2-2-6 ambapo mabeki wa pembeni husogea kwenye mstari wa mwisho usawa wa wale wanne wa mbele lengo likiwa ni mabeki wa pembeni kuongeza idadi wakicheza zaidi kwenye mapana ya uwanja ili kufungua nafasi kwenye mstari wa mwisho wa walinzi w timu pinzani na kurahisisha utengenezaji wa nafasi.

 

 

Silaha yao kubwa ni namna viungo wao washambuliaji wanvyopokea mipira katikati ya mistari, mfano Ryan Mendes akipokea jumla ya mipira 151 katikati ya mistari/nyuma ya mistari ya uzuiaji ya wapinzani huku 35 katikati ya mistari ya walinzi na mabeki na Kutoa pasi 1 ya goli huku akipiga mashuri 6 yaliyolenga lango, pia ubora wa utengenezaji wa nafasi hasa kwa Krosi mfano Lopes Cabral aliyepiga krosi 11.

 

 

Mfano mzuri wa moment hii ni goli la pili walilofunga dhidi ya Argentina linaloonyesha mtiririko wa mbinu kuanzia namna wanavyojenga shammbulizi na kuliendeleza kwenye theluthi zao mbili za mwanzo za uwanja na kisha namna wanavyopenya kuta za wapinzani wao na kutengeneza nafasi kwenye theluthi mbili mwisho, goli lililofungwa na Lopes Cabral.

 

Timu ikiporwa umiliki wa mpira (Defensive Transitions)

 

Cape Verde ikiporwa umiliki wa mpira hufanya mambo matatu kwa haraka ili kuzuia wapinzani wao kufanya shambulizi la kujibu kabla hawajarejea kwenye umbo lao zuri la kuzuia;

 

- Wachezaji huanza kuzuia presha na umakini mkubwa pale wanapopotezea mpira (Counter Pressing) huku mchezaji anayeongoza mara nyingi kuweka presha pale wanapopotezea mpira akiwa Deroy Duarte akifanya hivyo mara 137.

 

- Mara zote mpira ukiwa kwenye nusu ya wapinzani huwa umbo zuri kwenye mistari yao miwili ya mwisho linaloweza kumeza shambulizi la kujibu la wapinzani huku likiwa na mchezaji mmoja wa ziada kutengeneza faida ya idadi (Rest Defense) .

 

 

- Pia wachezaji hurudi kwa kasi kwenye maeneo yao kwaajili ya kudumisha umbo au mfumo mama wa kuzuia (4-1-4-1)

 

Mfano kwenye mchezo dhidi ya Argentina, goli lao la pili lilitokana na wachezaji kuanza kuzuia pale wanapopotezea Mpira kisha kuwalazimisha Argentina kupiga mpira kwa mshambuliaji wao mmoja wa mbele aliyekuwa dhidi ya mabeki wawili wa Cape Verde (2v1) wakameza shambulizi la kujibu kwa kupora mpira kisha wakaurudisha mbele na kupata goli.

 

Mipira ya kutenga (Set Plays)

Kwenye moment hii Cape Verde hawakuwa na makali sana kwani licha ya kupata Kona 17 na Freekick 57 ni goli 1 tu ndilo limetokana na moment hii ambalo ni la Freekick huku wakiruhusu kufungwa goli moja la kona dhidi ya Argentina.

 

Hitimisho

Mbinu za Kocha Pedro Leitão Brito ‘Bubista’ zimethibitisha kuwa licha ya kuwa na kikosi cha wachezaji wa Ubora wa daraja la kati lakini wanaweza kusukwa kimbinu na kutengeneza timu inayoweza kushindana kiwango cha dunia kama Cape Verde ilivyoonyesha kwenye kombe la dunia.

Pia anathibitisha kuwa hakubahatisha kuwa kocha bora wa tuzo za Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) mwaka 2024 ambapo aliiwezesha Cape Verde kufika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON)

 

 

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet