CAF waomba radhi kisa mechi ya Berkane kuahirishwa
Sisti Herman
April 22, 2024
Share :
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeomba radhi wadau wa soka baada ya mechi ya kwanza ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho kutofanyika baada ya klabu ya RS Berkane kususa.
Vigogo hao wa Morocco waliamua kuondoka uwanjani muda mfupi kabla ya mechi hiyo baada ya mamlaka nchini Algeria kuizuia kutumia jezi zao zenye ramani ya Morocco inayojumuisha eneo lenye mgogoro wa kisiasa.
Awali CAF iliagiza mamlaka nchini Algeria iwarejeshee RS Berkane jezi hizo, lakini timu ilipofika vyumba vya kubadilishia nguo haikuzikuta na ndipo ikaamua kugeuza na kuondoka uwanjani.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye tovuti yake, CAF imesema suala hilo litapelekwa kwenye chombo kinachohusika kwa ajili ya uamuzi.
CAF imewaomba radhi mashabiki, wadhamini, watangazaji na wengine wote walioathiriwa na tukio hilo.