Cancelo awashangaa wanaosahau makubwa ya Ronaldo na Neymar
Eric Buyanza
June 23, 2026
Share :

Beki wa Ureno João Cancelo amesema si Cristiano Ronaldo wala Neymar wanaostahili ukosoaji kwa hivi sasa kwenye Kombe la Dunia.
Ronaldo alikashifiwa na vyombo vya habari baada ya kufanya vibaya katika mchezo wa kwanza wa Ureno ilipotoa sare ya 1-1 na Congo DR, huku Neymar akiwa hajacheza mechi mbili za kwanza kutokana na jeraha la mguu ambapo wakosoaji wanahoji ni kwanini alijumuishwa kwenye kikosi.
“Vipaji vyao na kile ambacho wamefanikiwa katika soka vinajieleza.
Cristiano na Neymar wanajua wao ni nani na wanawakilisha nini kwa nchi zao.”alisema Cancelo.
Ronaldo alijiunga na nahodha wa Argentina Lionel Messi kama wachezaji pekee walioshiriki Kombe la Dunia mara sita ingawa bado hajaona nyavu.
Nahodha huyo wa Ureno ndiye mfungaji bora wa muda wote kwa Ureno, akiwa amefunga mabao 143 tangu acheze kwa mara ya kwanza katika timu yake ya taifa mwaka 2003.
Neymar ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Brazil akiwa na mabao 79 katika mechi 128 alizocheza.





