Chadema Ubungo wakamilisha ujenzi wa ofisi
Sisti Herman
June 23, 2024
Share :
Meya wa zamani Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, Boniface Jacob amesema Chama cha Demokrasia (Chadema) Wilaya ya Ubungo imejipanga kuibuka kidedea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 2024 kutokana na maandalizi wanayoendelea kuyafanya.
Miongoni mwa maandalizi hayo ni kukamilika kwa ofisi ya Jimbo ya Ubungo huku Kibamba mchakato ukiendelea. Ofisi hizo zitatumika katika kuratibu shughuli za uchaguzi huo kwa nyakati tofauti.
Jacob aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, amesema hayo leo Jumapili, Juni 23, 2024 wakati akikabidhi ofisi ya Jimbo la Ubungo, baada ya kumalizia ujenzi wake ulioanzia Mei 12, 2024.
"Nguvu ya Chadema kushinda mitaa 47 ya Ubungo ipo kutokana na kuwa na timu nzuri ya wilaya na kata itakayowezesha ushindi wa mitaa. Tuna wanachama wa Chadema walio tayari kupambania ushindi wa Chadema," amesema Jacob.
Jacob maarufu Boni Yai amesema haoni sababu ya Chadema kushindwa kuinyakua mitaa 47 ya wilaya hiyo, kutokana na uwepo wa vitendo kazi ikiwemo ofisi mpya ya kisasa ya maandalizi ya mchakato huo.
"Mimi na wanachama wenzangu tulichokifanya ni kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kisasa ili iwe ngome ya ushindi kuanzia Serikali za mitaa. Sasa tunachowaidai viongozi wetu ni matokeo ya Serikali za mitaa, nataka ofisi itumike hadi kwa ajili ya mikutano.
"Tuna deni kubwa la kukomboa mitaa yetu 47 ya Jimbo la Ubungo iliyokwenda chama tawala cha CCM," amesema.
Kuhusu ujenzi wa ofisi hiyo Jacob amesema:"Nilichokifanya nimemalizia sehemu ya ujenzi wa ofisi maana kwa muda mrefu ilikuwa kama boma, viongozi wa jimbo walinifuata na kuniomba nishiriki mchakato.